Wengine husema aah! Hiyo ni sehemu ya kufikirika na hakuna kitu kama hicho, na wengine husema ukifa ndio mwisho hakuna kinachoendelea, wengine husema Siku ukifa unaenda mbinguni na maneno mengine chungu mzima. Sasa hakuna mwanadamu anayejua haya ila Mungu.. Mungu katika neno lake ametoa maelekezo.
1. Je, Mbinguni Ni Mahali Halisi?
Yesu anatuandalia sisi mahali halisi kabisa hivi sasa katika mbingu iliyo ya halisi kabisa."Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi [Yesu]. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi kama sivyo, ningaliwaambia. Naenda KUWAANDALIA MAHALI. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, NITAKUJA TENA, niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo." - Yohana 14:1-3, KJV.
Yesu anakuja mara ya pili katika dunia yetu hii ili kutuchukua kwenda kwenye makao yaliyoandaliwa kukidhi utashi wa kila mtu katika mji wa mbinguni ulio na utukufu upitao ndoto zetu zote zilizochanganyikiwa mno; yaani, Yerusalemu mpya.
Je, Yohana, aliyekiandika kitabu cha Ufunuo, anatoa picha gani nyingine?
"Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule Mtakatifu, Yerusalemu Mpya ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi - arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi, ikisema, 'Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye ataisha pamoja nao. Watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao na kuwa Mungu wao" - (Ufunuo 21:1-3).
2. Je, Tutakuwa Na Miili Halisi Mbinguni?
Yesu alipowatokea wanafunzi wake akiwa na mwili wake uliofufuka na kutukuzwa, je, aliuelezaje mwili ule?"Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa, kama mnavyoniona mimi kuwa nayo" - (Luka 24:39).
Yesu alikuwa na mwili halisi; alimtaka Tomaso amguse (Yohana 20:27). Wakati ule Yesu alitembea na kuingia katika nyumba halisi, na kuzungumza na watu halisi, na kula chakula halisi (Luka 24:43).
Kule mbinguni hakukaliwi na roho, bali na watu halisi wanaoyafurahia maisha ya kiroho, na ambao wana "mwili.. wa utukufu."
Nasi kwa hamu kubwa tunamngojea Mwokozi wetu kutoka kule, yaani, Bwana Yesu Kristo, ambaye, kwa uweza wake unaomfanya kuvidhibiti vitu vyote chini yake, ataibadilisha miili yetu hii minyonge ili ipate kufanana na mwili wake wa utukufu" - (Wafilipi 3:20,21).
Tunaweza kuwa na hakika kwamba miili yetu ya mbinguni itakuwa imara na ya kweli kweli kama ulivyokuwa mwili wa Kristo aliyefufukwa.
Je, tutaweza kuwatambua watu wa familia yetu pamoja na marafiki zetu kule mbinguni?
"Tuanachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi - (1 Wakorintho 13:12).
Kule mbinguni tutajua sana." Tutaelewana na kuthaminiana kwa kina kuliko tulivyopata kufanya katika dunia ya sasa.
Wanafunzi wa Yesu walimtambua akiwa katika mwili wake wa mbinguni, ni dhahiri kutokana na sura yake walipokuwa wamezoea kuiona (Luka 24:36-43).
Fikiria furaha utakayokuwa nayo ukiitambua tabasamu ya aina yake ya mume au mke wako, au sauti inayokuita ambayo kwako inafahamika ya mtoto wako uliyemlaza kaburini zamani sana, ishara za mikono zinazoonyesha upendo kwako za rafiki yako fulani mpendwa wako.
3. Tutafanya Nini Kule Mbinguni?
Tutakuwa na shughuli nyingi za kutupatia changamoto kule mbinguni. Vipi kama wewe utaibuni mwenyewe nyumba yako unayoiwazia?"Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya… Nami nitafurahia Yerusalemu, na kuwaonea shangwe watu wangu… Watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mashamba ya mizabibu, na kula matunda yake… Wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi" - (Isaya 65:17-22).
Tayari Yesu anaandaa nyumba zetu binafsi katika ule Mji Mtakatifu, yaani, Yerusalemu Mpya (Yohana 14:1-3; Ufunuo 21). Mafungu hayo yanadokeza kwamba sisi pia tutabuni nakuzijenga nyumba nyingine - huenda zikawa ni zile nyumba zetu nzuri za mashambani, ambazo tutaziwekea mandhari nzuri sana ya mimea hai mbalimbali.
Mungu ataigeuza nchi hii itakuwa kama Bustani ya Edeni ya zamani. Hakuna tena kumwagika ovyo ovyo kwa mafuta, wala mchanganyiko wa ukungu na moshi, wala ukame; maziwa yatakuwa safi kama kioo, miti itakuwa na fahari yake, na mitelemko ya milima itakuwa bila waa lolote.
4. Je! Uovu Utaitishia Mbingu Tena?
"Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo" - (Ufunuo 21:27).Mungu ataiondoa kabisa dhambi pamoja na athari zake za kutisha; mambo hayo hayataonekana tena. Yesu atakapoonekana, "tutafanana naye" (1 Yohana 3: 2). Badala ya kuipiga misukumo iliyo ndani yetu ya kuua, kuiba, kusema uongo, au kubaka, sisi tutaendelea kuwa na zile tabia nzuri za mbinguni.
"Naye [Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakauwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo, kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita"- Ufunuo 21:4.
5. Je, Furaha Kuu Kuliko Zote Mbinguni Ni Ipi?
Hebu fikiria kwamba wewe unamwona Bwana wa malimwengu uso-kwa-uso."Tazama maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maisha yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao, naye atakuwa Mungu wao" - (Ufunuo 21:3).
Mungu mwenyezi anaahidi kwamba atakuwa mwenzi na mkufunzi wetu. Ni furaha iliyoje hiyo kukaa miguuni pake!
"'Na itakuwa mwezi mpya hata mwezi mpya, na Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, 'asema BWANA" - (Isaya 66:23).
6. Huna budi kuwa Kule!
Yesu anatamani sana kukutana nasi uso kwa uso wakati ule. Ndiyo maana yeye alipenda kukuokoa wewe kutoka katika dhambi kwa gharama kubwa kama ile. Wewe binafsi ni lazima unufaike kwa kuipokea zawadi hiyo. Ni lazima wewe ujitoe kabisa kwake Kristo awe Bwana na Mwokozi wako. Unahitaji msamaha wake unaotolewa kwako kutoka katika ule msalaba, kwa sababu: "Ndani yake kamwe hakitaingia cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo ya uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo" - (Ufunuo 21:27).Yesu anatuokoa kutoka katika dhambi [uvunjaji wa Amri Kumi], sio pamoja na dhambi [uvunjaji wa Amri Kumi]. Yatupasa kuja kwake kwa uwezo wake ulio ndani yetu na kutengwa mbali na uchafu na uovu. Yesu ni neno letu kuu la kuingilia katika ufalme wake unaokuja upesi.
Na ufalme ule unaweza kuanza sasa hivi ndani ya moyo wako. Kristo anapotuokoa sisi kutoka katika dhambi, anaiweka mbingu ndogo ndani ya moyo wetu.
Anaweza kutusaidia sisi katika kushughulikia wasiwasi, hasira, tamaa ya mwili, hofu, na hatia inayotusumbua. Tumaini la kwenda mbinguni si njia ya kuyakwepa matatizo yanayotukabili katika maisha yetu; linasaidia kuileta mbingu kwa wingi zaidi hapa duniani. Kura iliyopigwa hivi karibuni ilionyesha kwamba "wale wanaoamini kwamba maisha yatakuwako baada ya kifo walikuwa na maisha yenye furaha na kuwa na imani na watu kuliko wale wasiosadiki hivyo."
Hakuna kitu cho chote kitakachokuwa na mvuto unaosisimua sana katika maisha yako ya wakati huu wa sasa kama kuwa na uhusiano wa imani na Yesu Kristo. Hebu sikiliza jinsi Petro anavyoeleza matokeo ya imani iliyo hai: "Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka yenye utukufu, katika kumpokea mwisho wa imani yenu, yaani wokovu wa roho zenu" - (1 Petro 1:8,9).
Yote hayo utapata - pamoja na mbingu pia. Je! wewe umekwisha kugundua aina ile ya maisha tele ambayo Kristo anataka wewe uwe nayo? Tafadhali usigeuke na kwenda zako kwa kuukataa mwaliko wake huu wa neema.
"Na Roho na Bibi-arusi, wasema, 'Njoo!' Naye asikiaye na aseme, 'Njoo!' Naye mwenye kiu, na aje; na ye yote atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure" - (Ufunuo 22:17).
Yesu yu pamoja nawe hivi sasa, anazungumza na moyo wako unaposoma mistari hii. Anakualika wewe, anasema, "Njoo!" "Njoo!" "Njoo!" Asingeweza kuwa na shauku kubwa zaidi ya hiyo, asingesisitiza zaidi ya hivyo alivyokwisha kufanya. Kama wewe bado hujafanya hivyo, basi, hii ndiyo dakika yako ya kukichunguza kipawa chake hicho.
Kwa nini wewe usimwambie ya kwamba unakubali kukipokea kipawa chake hicho cha neema yake na ya kwamba wewe unataka kuishi milele pamoja naye? Mwambie kwamba wewe unampenda. Umshukuru kwa yote aliyokutendea na kwa yale ambayo unapanga kwa ajili yako.
Kama kuna kitu cho chote kati yako na Mungu, basi, mwombe akufanye upende kuachana nacho. Leo hii, unapoisikia sauti yake, wakati moyo wako bado unavutwa kwake, jitoe kwake wewe mwenyewe bila kuacha kitu. Inamisha kichwa chako dakika hii na kusema, "Yesu, Bwana wangu, naja kwako. Nakupa wewe vyote nilivyo navyo. Mimi nataka kuwa wako milele hata milele.
Je, unatamani kujua zaidi kuhusu neno la Mungu?
Wasiliana Leo
Dr Nature
0767759137
real.dr.nature@gmail.com


























